Swahili New Testament Bible

1st Timothy 5

1 Timothy

Return to Index

Chapter 6

1

 Watumwa wote wanapaswa kuwaheshimu wakuu wao ili kusiwe na sababu ya watu kulitukana jina la Mungu na mafundisho yetu. 


2

 Watumwa ambao wakuu wao ni Wakristo wasiwadharau kwani ni ndugu zao. Badala yake, wanapaswa kuwatumikia hata vizuri zaidi, maana hao wanaopata faida kutokana na kazi yao ni waumini ambao wanawapenda. Unapaswa kufundisha na kuhubiri mambo haya. 


3

 Mtu yeyote anayefundisha kinyume cha mambo haya, na ambaye hakubaliani na maneno ya kweli ya Bwana wetu Yesu Kristo na mafundisho ya dini, 


4

 huyo amejaa majivuno na wala hajui chochote. Ni mtu wa kupenda ubishi na magombano juu ya maneno matupu, na hiyo husababisha wivu, ugomvi, matusi, shuku mbaya, 


5

 na ubishi usio na kikomo kutoka kwa watu ambao akili zao zimeharibika, na ambao hawana tena ukweli. Wanadhani dini ni njia ya kujipatia utajiri. 


6

 Kweli dini humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo. 


7

 Maana hatukuleta kitu chochote hapa duniani, wala hatutachukua chochote. 


8

 Kwa hiyo basi, kama tunacho chakula na mavazi, tunapaswa kuridhika navyo. 


9

 Lakini wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi. 


10

 Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote. Watu wengine wametamani sana kupata fedha hata wakatangatanga mbali na imani, na wameivunja mioyo yao kwa huzuni nyingi. 


11

 Lakini wewe, mtu wa Mungu, jiepushe na mambo hayo. Zingatia uadilifu, uchaji wa Mungu, imani, mapendo, subira na unyenyekevu. 


12

 Piga mbio kadiri uwezavyo katika shindano la mbio za imani, ukajipatie tuzo la uzima wa milele, uliloitiwa wakati ulipokiri imani yako mbele ya mashahidi wengi. 


13

 Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato, 


14

 nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka Siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo. 


15

 Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. 


16

 Yeye peke yake anaishi milele, katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina. 


17

 Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie. 


18

 Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao. 


19

 Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uzima ambao ni uzima wa kweli. 


20

 Timotheo, tunza salama yote yale uliyokabidhiwa. Jiepushe na majadiliano ya kidunia na ubishi wa kipumbavu juu ya kile wanachokiita watu wengine: "Elimu". 


21

 Maana wengine wamejidai kuwa na hiyo elimu, na matokeo yake wamepoteza imani. Nawatakieni nyote neema! 


2nd Timothy 1

 

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: