| Chapter 4 |
1 | Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.
|
2 | Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.
|
3 | Ndipo Ibilisi akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate."
|
4 | Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Mtu haishi kwa mkate tu."`
|
5 | Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,
|
6 | "Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.
|
7 | Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu."
|
8 | Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake."`
|
9 | Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, "Kama wewe ni Mwana wa Mungu,
|
10 | kwa maana imeandikwa: `Atawaamuru malaika wake wakulinde,`
|
11 | na tena, `Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe."`
|
12 | Lakini Yesu akamjibu, "Imeandikwa: `Usimjaribu Bwana Mungu wako."`
|
13 | Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.
|
14 | Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.
|
15 | Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.
|
16 | Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.
|
17 | Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
|
18 | "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,
|
19 | na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana."
|
20 | Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.
|
21 | Naye akaanza kuwaambia, "Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo."
|
22 | Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, "Je, huyu si mwana wa Yosefu?"
|
23 | Naye akawaambia, "Bila shaka mtaniambia msemo huu: `Mganga jiponye mwenyewe`, na pia mtasema: `Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako."`
|
24 | Akaendelea kusema, "Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.
|
25 | Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
|
26 | Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.
|
27 | Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria."
|
28 | Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.
|
29 | Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
|
30 | Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
|
31 | Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
|
32 | Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
|
33 | Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
|
34 | "We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!"
|
35 | Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: "Nyamaza! Mtoke mtu huyu!" Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
|
36 | Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, "Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!"
|
37 | Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.
|
38 | Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.
|
39 | Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.
|
40 | Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.
|
41 | Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: "Wewe u Mwana wa Mungu!" Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.
|
42 | Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.
|
43 | Lakini yeye akawaambia, "Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo."
|
44 | Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.
|