Swahili New Testament Bible

Revelation 4

Revelation

Return to Index

Chapter 5

1

 Kisha katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nikaona kitabu; nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na mihuri saba. 


2

 Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: "Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?" 


3

 Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini Kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani. 


4

 Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani. 


5

 Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, "Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu." 


6

 Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo amesimama, akizungukwa kila upande na vile viumbe hai vinne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani. 


7

 Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. 


8

 Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja, alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu. 


9

 Basi, wakaimba wimbo huu mpya: "Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa. 


10

 Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu nao watatawala duniani." 


11

 Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, vile viumbe hai vinne na wale wazee; 


12

 wakasema kwa sauti kuu: "Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa." 


13

 Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na baharini--viumbe vyote ulimwenguni--vikisema: "Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi milele na milele." 


14

 Na vile viumbe vinne hai vikasema, "Amina!" Na wale wazee wakaanguka kifudifudi, wakaabudu. 


Revelation 6

 

 

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: